Wanazuoni, wasomi na viongozi wa dini mbalimbali wakutana jijini kujadili dhana ya Mkombozi kama kiungo cha pamoja cha imani na bishara ya mustakabali mwema wa wanadamu.

13 Februari 2026 - 23:15

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam - Tanzania, Leo Ijumaa, 13 Februari 2026 - Uwakilishi wa Kieneo wa Jamiat Al-Mustafa Al-Alamiya – Tanzania umefanya Kikao cha Tano cha Kielimu chenye mada isemayo: “Mkombozi katika Mawazo ya Dini: Tumaini la Viumbe Wote.” Kongamano hilo limewakutanisha washiriki kutoka dini na madhehebu mbalimbali kwa lengo la kuchambua nafasi ya dhana ya Mkombozi katika imani za wanadamu.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wanazuoni, wasomi, wanafikra pamoja na watu mashuhuri kutoka dini tofauti, ambao waliwasilisha hotuba za kitaaluma zikijikita katika fikra ya kumngojea Mkombozi wa Ulimwengu - dhana inayopatikana katika mafundisho ya dini nyingi duniani. Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi kupitia Hotuba ya ufunguzi aliyoitoa Rais wa Jamiatul - Mustafa (s) - Tanzania, Dr.Ali Taqavi.

Wahadhiri Waliotoa Mada

Miongoni mwa wahadhiri waliopamba kongamano hilo kwa mara zao maridadi ni pamoja na:

1_Mheshimiwa Himmat Panah, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Nchini Tanzania.

2_Dr. Sheikh Al-Hadi Musa Salum - Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), aliyesisitiza umuhimu wa dhana ya Mkombozi katika kujenga maelewano, amani na mshikamano wa kitaifa na kimataifa.

3_Mr. Pirthpal Singh Sanghera - Mfuasi wa Dini ya Sikh, aliyeeleza mtazamo wa imani yake kuhusu matumaini ya wokovu na uongozi wa kiroho katika zama za mwisho.

4_Dr. Ali Dina - Aliyetoa uchambuzi wa kina kuhusu nafasi ya itikadi ya Mkombozi katika kuimarisha maadili na mshikamano wa kijamii.

5_Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge - Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania - T.I.C.

6_Dr. Christosiler Petro Kalata - (Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Dar-es-salaam) na Mfuasi wa Dini ya Ukristo, aliyeangazia dhana ya Masihi kama tumaini la ukombozi wa kiroho na kijamii.

7_Sheikh Ali Khamis Ngeruko - Kaimu Mufti wa Tanzania.
 

Mkombozi kama Kiungo cha Pamoja
Kwa ujumla, wahadhiri walikubaliana kuwa dhana ya Mkombozi ni kiini kinachoweza kuziunganisha dini mbalimbali, kwani inabeba ujumbe wa matumaini, haki na ushindi wa wema dhidi ya uovu. Walieleza kuwa matarajio ya ujio wa Mkombozi si tu suala la kiitikadi, bali pia ni msukumo wa kimaadili unaochochea juhudi za kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Washiriki walihimiza kuendelezwa kwa majadiliano ya kielimu na kidini ili kukuza uelewano baina ya jamii tofauti, wakisisitiza kwamba imani ya Mkombozi ni bishara njema ya mustakabali mwema kwa ubinadamu wote.

Kongamano hilo limeonekana kuwa jukwaa muhimu la kukuza mazungumzo ya kidini na kuimarisha mshikamano wa kijamii kupitia misingi ya imani na matumaini ya pamoja.

Your Comment

You are replying to: .
captcha